KIJANA CHACHU YA MAENDELEO
Maendeleo ni moja ya kiashiria muhimu wakati wa utekelezaji wa Dira na Dhamira ya KIYOA. Kwa mujibu wa KIYOA, "Maendeleo" ni "hali ya mtu au kundi la watu kufanikiwa kiuchumi na kijamii". Aidha, kufanikiwa kiuchumi inahusisha hali ya kujiongezea kipato kwa njia za halali wakati kufanikiwa kijamii inahusisha kuishi maisha shirikishi ambayo jamii inaweza kutatua changamoto inazozikabili kwa kupitia ushiriki wa watu wake wakati wa kutatua changamoto husika.
Kimsingi, kuna changamoto nyingi zinazowakabili watu katika jamii zao, vile vile changamoto hizi hutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine. Mfano, jamii moja wakati inakabiliwa na ujinga, elimu duni, maradhi, n.k, wakati huo huo jamii nyingine inakabiliwa na majanga kama vile vita vya wenyewe kwa wenyewe, mafuriko ya maji, vimbunga, matetemeko ya ardhi, n.k.
Katika baadhi ya maeneo hapa nchini, jamii zetu zimekuwa zikikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa ni vikwazo vya maendeleo katika maeneo husika. Baadhi ya changamoto hizi ni pamoja na utumiaji wa madawa na kulevya, maradhi mbalimbali, uharibifu wa mazingira, uwezo mdogo wa kujikimu kimaisha, ufinyu wa bajeti katika kutekeleza mipango ya maendeleo, n.k.
Pamoja na jitihada zinazochukuliwa na Serikali ikiwemo kutoa elimu katika kupambana na changamoto husika, mwamko mdogo kwa baadhi ya Wanajamii hususan vijana (nguvukazi ya taifa la leo) katika kujitoa kushiriki kikamilifu kusaidiana na jamii ni moja ya changamoto kubwa ndani ya jamii zilizo nyingi, changamoto hii imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa jamii husika katika kujiletea maendeleo endelevu kupitia njia ya kujitolea.
Ili tuweze kutimiza azma ya "Maendeleo Endelevu" kwa taifa letu, ni vyema vijana sasa popote tulipo tujiunge pamoja katika vikundi vya kijamii na kutumia ujuzi, taaluma na sehemu ya muda tulionao katika kisaidia juhudi za maendeleo katika jamii zetu tunazoishi.
Vijana ni vyema tukafahamu kuwa, sote kwa pamoja tuna jukumu kubwa katika kujenga jamii bora kwa kutumia sehemu ya muda wetu, ubunifu, ujuzi , taaluma na elimu tulizonazo kwa kuwa "Vijana ni Chachu ya Maendeleo katika Jamii Tunazioshi."
VIJANA TUKIAMUA!! TUNAWEZA!!